Kauli ya Yondani baada ya Viongozi wa Yanga Kumfwata
WA siku kama tano hivi, beki na nahodha msaidizi wa Yanga, Kelvin Yondani ‘Vidic’ aliwapa presha mabosi wake wa Jangwani sambamba na wanachama wa klabu hiyo.
Hii ni kutokana na kuamua kuwazimia simu, jambo lililowafanya mabosi wake kufanya msako wa nyumba kwa nyumba ili kumpata wajue tatizo lake.
Juzi Jumamosi mabosi hao walipata mawasiliano ya beki huyo na asubuhi ya jana Jumapili waliamua kutimba nyumbani kwake Toangoma, Kigamboni pembezoni mwa
jijini la Dar es Salaam na beki huyo kufichua mengi ikiwamo kuzitaja klabu za Azam na Simba kuwa ndio tatizo lililomfanya aamue kukata mawasiliano.
Pia Yondani aliamua kuwashusha presha mabosi wake hao kwa kuwaambia kitu flani kitamu hata kukisikia masikioni mwa Wanayanga wanaomzimia kwa kazi yake uwanjani.
UJUMBE MZITO
Mabosi wa klabu hiyo walilazimika kufunga safari ndefu mpaka nyumbani kwa beki huyo, Katibu wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Samuel Lukumay aliongoza msafara huo akiambatana na mjumbe wa kamati hiyo, Lucas Mashauri na mwanachama Edwin Kaisi. Ujumbe huo ulitimba kwa Yondani na kukutana naye sambamba na meneja wake, Peter Sosthenes ‘Mourinho’ na baada ya kukaribishwa ndani walianza mazungumzo.
YONDANI ALONGA
Katika mazungumzo hayo Yondani aliwaambia mabosi wake kuwa kukaa kwake kimya kulitokana na kukwepa usumbufu wa sakata lake la mkataba mpya ambapo simu za mabosi wa Simba na Azam zilikuwa hazikauki kwake.
Yondani alisema kutokana na hilo aliamua kuzima simu zake akisubiri mazungumzo yake na Yanga yanafikia wapi juu ya kuongeza mkataba mpya. Beki huyo mkongwe nyuma kidogo ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema hana nia ya kutaka kuondoka Yanga na kwamba tayari ameshazungumza na familia yake na meneja wake, lengo lake ni kumalizia soka lake Yanga kama watakubaliana mkataba mpya.
MSIKIENI WENYEWE
“Unajua viongozi wangu niwaambie ukweli akili yangu ilikuwa haijatulia mambo yalikuwa mengi huku haya mambo ya TFF (Sakata la lake na beki wa Simba Asante Kwasi) hayajatulia lakini mambo ya mkataba mpya nayo yanaingia,” alisimulia.
“Unajua kama tulivyozungumza jana (juzi) kwa simu mimi niliumia katika mechi ya Simba nikaona nitulie ili nipone vizuri hii habari ya kucheza huku unaumwa inaweza kuleta shida, changamoto ikaja juu ya matibabu nashukuru Mungu niko sawa kidogo.
“Sasa nikiwa hapa mambo ya kutakiwa na Simba na Azam yakaibuka, simu zao zilikuwa nyingi sana hasa watu wa karibu na viongozi wa timu hizo, nikaona isiwe tabu nikazima simu kwanza akili yangu ni kubaki Yanga, sio kuondoka. Walikuwa wanapiga sana simu ingawa hawakunitajia kiasi gani watanipa.
“Niwaambie ukweli sitaki kuondoka Yanga kama tutakubaliana nataka soka langu nimalizie hapa, nataka nikistaafu nistaafu kwa heshima sio mpaka nifukuzwe lakini itategemea kama tutafikia wapi katika mazungumzo haya.”
AWAONYA MABOSI
Yondani alienda mbali kwa kuwaambia mabosi wake kuwa, licha ya kikosi chao kwa sasa kikishiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ila wanatakiwa kuunda vyema timu yao baada ya kupata Kocha Mwinyi Zahera.
Alisema ndani ya kikosi cha sasa kuna upungufu katika baadhi ya idara na lazima mambo yawekwe sawa ili timu itishe zaidi.
Yondani alisema wakati mwingine amekuwa yeye na wenzake wanajikuta wakifanya rafu zisizo na maana kutokana na upungufu huo.
“Timu yetu sio mbaya lakini mkikaa na makocha watawaeleza binafsi kutokana na ukongwe wangu katika timu hii kuna maeneo lazima muyafanyie usajili na kuleta wenye uwezo.
“Unajua kuna wakati watu wanaweza kutuona kama tunafanya mambo ya ajabu kwa kucheza rafu lakini pia inatokana na kuzidiwa uwanjani sasa maoni yangu tulieni mtengeneze timu nzuri, msiwe na wasiwasi nami timu ikirudi nitajiunga nayo. “Nawashukuru sana kwa kuja kuniona ni viongozi wachache wanaweza kujitoa na kuja kuwaangalia wachezaji wao.”
KAULI YA MABOSI
Kwa upande wa Lukumay aliye pia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, alisema amefurahishwa kusikia msimamo wa beki huyo na sasa wako katika hatua za mwisho kumaliza ishu ya mkataba wake mpya.
Lukumay alisema uongozi ulishtushwa na taarifa za Yondani anataka kuhama timu hiyo wakiona ni tofauti na hatua ya mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea.”
No comments