SIMBA v/s YANGA MWEZI UJAO
MECHI ya watani wa jadi Simba na Yanga ambayo ilikuwa ichezwe Aprili 7 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam sasa itachezwa Aprili 29.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPBL), Boniface Wambura amesema wamefanya mabadiliko ya ratiba kwa mechi kadhaa kwa sababu wanataka Ligi Kuu imalizika Mei 26 kama ilivyopangwa.
"Ratiba imebana sana hivyo mchezo wa kiporo wa Njombe na Simba utachezwa Aprili 3 na tumefanya kazi ya ziada kukubaliana na Njombe kwani wanasema ratiba siyo rafiki kwao lakini nashukuru wametuelewa," alisema Wambura.
Pia Wambura alisema mchezo wa Simba na Yanga utachezwa Aprili 29 badala ya Aprili 7 ili kuipa Yanga nafasi kujiandaa na mchezo wa kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Wolayta Dicha ya Ethiopita unaotarajiwa kuchezwa Aprili 4 kwenye uwanja wa Taifa.
Mechi ya Simba na Yanga inatarajiwa kuwa ya vuta nikuvute hasa kwa vile timu hizo zimeonesha upinzani mkubwa kileleni mwa msimamo na hivyo mpaka sasa yeyote kati yake anaweza kuwa bingwa. Simba inaongoza msimamo kwa uwiano mzuri wa mabao baada ya kulingana pointi 46 na Yanga iliyo nafasi ya pili.
Wambura amesema, ratiba hiyo inaweza kufanyiwa tena marekebisho endapo Yanga itafuzu kwenye hatua ya makundi huku akisema sababu nyingine zinazofanya ratiba kupanguliwa ni kutokana na timu kutokuwa na viwanja vyao hivyo wamiliki wa viwanja wanapokuwa na shughuli za kijamii mechi zinasogezwa mbele.
Mechi nyingine zilizofanyiwa marekebisho ni Mbao dhidi ya Lipuli utakaochezwa Aprili 6 na tarehe hiyo tena Mwadui Shinyanga. Mtibwa Sugar itacheza na Simba Aprili 9 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Yanga itacheza na Stand United Aprili 11, Simba itaivaa Mbeya City Aprili 12 na Aprili 16 itaikaribisha tena Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Taifa.
Lipuli itakuwa mwenyeji wa Simba Aprili 20 na Majimaji itacheza na Ruvu Shooting Aprili 28. Wambura alisema wamepata kibali cha kutumia uwanja wa Taifa kwa michezo inayohusu Simba na Yanga isipokuwa mchezo wa Yanga dhidi ya Azam FC utalazimika kuchezwa kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
No comments